February 10 mwaka huu nilisikiliza kwa makini taarifa ya Ndugu Reginald Mengi, Mwenyekiti Mtendaji wa Makampuni ya IPP na Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Vyombo vya Habari (MOAT) hapa nchini kuhusu tuhuma alizotoa kwa watu wasiojulikana ambao anadai ni watuhumiwa wa ufisadi.
Katika taarifa yake Mengi alilalamikia magazeti anayodai kuwa yanafadhiliwa na watuhumiwa wa ufisadi kwa kuandika mambo yaliyojaa fitna na uongo dhidi yake na familia yake. Aidha alitaja pia baadhi ya tuhuma ambazo magazeti hayo yamekuwa yakiandika juu yake na kusema kuwa tuhuma hizo ni uongo.
Kilichonishangaza zaidi katika sakata hilo ni kesho yake baadhi ya vyombo vya habari kudai kuwa Bwana Mengi alikataa kutoa majibu kwa maswali ya waandishi wa habari kuhusiana na tuhuma hizo. Hali hiyo kwangu mimi naona ilikuwa na utata kwa sababu kama Mengi aliamua kuita waandishi awaeleze ukweli kuwa yale yaliyoandikwa ni uongo, alitakiwa kuthibitisha. Na kukataa kujibu maswali hayo mi kumenipa wasiwasi juu ya ama uongo au ukweli wa tuhuma hizo.
Nikakumbuka kuwa siku za hivi karibuni vyombo vya habari ambavyo vinamilikiwa na makampuni ya IPP vimekuwa vikiandika habari mbaya zidi ya wale ambao Mengi anawatuhumu sasa kuwa wameanzisha vyombo vya habari ili kuficha ufisadi wao. Kwa hesabu zangu za haraka haraka nikahisi huenda wako njia moja ila tu labda wamezidiana ujanja.
Hawa watu wanalichezea taifa hili mchezo mchafu sana wa ufisadi. Kwanza wamefisadi mali za umma na sasa wanatumia vyombo vya habari kufisadi fikra na utashi wa umma wa watanzania. Mi sitaki kuamini kuwa hawa watu ni wema kwa nchi hii hata kidogo. Lakini watu hawa wanalindwa na kubebwa na vyombo vya habari wanavyovimiliki pamoja na waandishi wanaowakumbatia.
Nasema magazeti haya yanafisadi fikra za watanzania kutokana na ukweli kwamba yanasomwa na watu wengi hasa mijini na huko ndiko mara nyingi tumekuwa tukiamini kuwa mawazo mapya yanapaswa kutokea. Kwa maana hiyo mafsadi hawa wakifanikiwa kuharibu fikra za watu wanaoishi mjini wanakuwa wameharibu kabisa fikra za asilimia kubwa za watanzania na hatujui bado lengo lao ni nini.
Ninachoshangazwa zaidi ni kwamba Mengi ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Vyombo vya Habari, kwa nafasi yake hiyo angeweza kabisa kumaliza suala hilo ndani ya chama hicho na kama hao anaowasema sio wanachama basi angelalamika lasmi kwa serikali ambayo kisheria ndio inayosajili magazeti hayo au kwa Baraza la Habari Tanzania (MCT) ambalo tumeona likishughulikia kesi mbalimbali zinazofikishwa hapo kwa umakini kabisa.
Lakini pia najiuliza mpaka haya yote yatokee katika taifa hili, wanaoruhusu uharamia huu kuendelea kushamiri ni sisi waandishi wa habari. Tumekuwa tukitumiwa na mafisadi hawa kufisadi fikra za watanzania. Sina uhakika inawezekana hata fikra zetu wameshazifisadi na tunaona ni sawa kwa haya tunayoendelea kuyafanya.
Mimi siamini kama mwandishi mwenye maadili ya kazi yake anaweza kutumika na watu hawa akijua kabisa ni mchezo wao wa kuchafuana na kukubali kuandika haya ambayo baadhi ya magazeti yanayoandika sasa. Na mbaya zaidi sioni kama sisi kama waandishi tunakemea hawa wanaotuharibia taaluma namna hii. Tunasubiri tu serikali ikilifungia gazeti tuandamane na kutangaza kuwa Uhuru wa vyombo vya habari unaingiliwa.
Mimi naamini serikali yetu ya Tanzania imetupatia Uhuru ambao mimi ningekuwa Mheshimiwa Rais naamini nisingeutoa Uhuru huo. Bahati mbaya hata udiwani sijaupata! Lakini tunautumiaje sasa Uhuru wenyewe?
Katika taarifa yake Mengi anasema kuna magazeti 15 yanafadhiliwa na mafisadi pekee na na ukijumulisha baadhi ya magazeti yake yanayoandika kwa staili hiyo unakuta kuwa yanakaribia magazeti 20 mengi yakiwa yanatoka kila siku kwa Kiswahili na Kiingereza.
Sinania ya kusema waandishi tusifanye kazi kwenye vyombo hivi vya habari, la hasha. Ninachosema tufanye kazi kwa kulingana na maadili ya kazi yetu hasa tukitilia maanani madhara yanayoweza kusababishwa na uandishi wa namna hii.
Waandishi wa habari tusipojiheshimu na kujithamini hawa mafisadi hawanatuheshimu na wataendelea kututumia kila siku katika michezo yao michafu. Mbaya zaidi anayeonekana sio fisadi ni mhariri na mwandishi ndio majina yenu yanatokea katika jarida lile na sio hao mafisadi ambao tunawakingia kifua.
Wakati kashfa zote hizi zikiandikwa na vyombo vya habari, sioni kama serikali inachukua hatua zinazostahili. Na sijajua serikali sasa inasemaje kwa tuhuma hizi kuwa kuna mafisadi au watu wanaolihujumu taifa kwa namna moja au nyingine ambao wanatumia vyombo vyao vya habari vibaya na mara nyingi kinyume na taratibu, maadili na sheria za taifa hili.
Nadhani sasa ni wakati muafaka kwa serikali kupitia upya sera, sheria na usajili wa vyombo vya habari hapa nchini. Nakumbuka kuna wakati serikali iliendekeza kuwa waandishi wa habari wawe na angalau Diploma na sijui hili lilifikia wapi na ni kwa kiasi gani linafuatiliwa. Ukute tunalaumu taaluma hii inapotoshwa kumbe waanindishi wengi ni makanjanja wanaoharibu taaluma hii.
Ushauri wangu kwa waandishi wenzangu ni kuwa wazalendo na wenye kuheshimu dhamira zetu. Kwa kutumika kuandika haya tunayoandika sasa hivi sijui kama tunajenga au tunabomoa. Mimi nadhani tunawajenga mafisadi na tunajibomoa wenyewe kama wanataaluma. Kuna baadhi ya habari zinazoandikwa mpaka mtu unajiuliza kama hili gazeti linamhariri au mtu yeyote anayeheshimika ndani yake, na mbaya zaidi ukifungua gazeti hilo unakuta majina yao yameandikwa.
Kwa sasa inakuwa ngumu kutenganisha gazeti la udaku na la kawaida. Maana gazeti ulilokuwa unajua kuwa la kawaida kesho tu unalikuta linaudaku yaani habari zinazotiashaka kama zina ukweli ndani yake, hazina chanzo cha habari na inaonekana kama ni ya kubuni buni vile.
Kama kabisa tumeshindwa kuwa wazalendo kwa taifa letu basi mi naomba tunaheshimu dhamira zetu. Hivi dhamira zetu hazitusuti tunapokuwa tunawasaidia mafisadi hawa kuwafisadi wananchi wa Tanzania.
Naomba nieleweke kuwa sina ugomvi na watu wanaopinga ufisadi hapa nchini, hata mimi napinga ufisadi. Lakini huu ufisadi wa fikra za umma unaodaiwa kutumika kupinga ufisadi wa mali za umma ndio ninaoupinga mimi. Huu ni mbaya zaidi kuliko ufisadi wa mali ya umma tena wakati mwingine kuliko hata uhaini. Kwa sababu umma ukishapunguziwa uwezo wa kufikiri, hautaweza tena kupanga mipango na kuitekeleza itakayoleta maendeleo au hata kudhibiti mali zake ambazo zimekuwa zikitafunwa na wajanja wachache.
Pia naamini kuwa huwezi kuufuta ufisadi mmoja kwa kutumia njia ambayo inaanzisha ufisadi mwingine. Naamini ufisadi unaweza kufutwa na dhamira ya kweli ya kupambana na ufisadi na sio dhamira ya kuwapumbaza wananchi wasijue ukweli pale unapohitajika.
Sitaki kuamini kama wataalamu wa wizara inayohusika hawajafikiria hili. Ifike mahali serikali ione sasa kwamba inatosha na ichukue hatua sitahiki. Isipochukua hatua inafanya baadhi ya watu tuamini kuwa hata yenyewe pia au imeathirika na huu ufisadi wa kifikra unaoendelea au baadhi ya wakubwa wake wanahusika na ufisadi huu wa fikra za umma au wa mali za umma.
Napenda pia kuwakumbusha Waandishi wa Habari Wanawake (TAMWA), Jukwaa la Wahariri, Baraza la Habari Tanzania, MISA Tanzania, vyuo vya vinavyojihusisha na taaluma ya uandishi wa habari na wadau wengine wote kutimiza wajibu wetu. Jamani na sisi pia tumeathirika na ufisadi huu? Mi sioni kama tunakemea vya kutosha au hata kuonyesha njia katika huu ufisadi unaoendelea. Au ni mimi tu ndio ninayeiona hali hii. au tuko wachache mmo na hatusikiki?
Wednesday, 11 February 2009
Subscribe to:
Posts (Atom)